HOME OF ACTIVE PEOPLE

Hi! welcome to Apex blog, home of active people. As you navigate through various pages and posts you will be able to enjoy our rich text. Remember to leave your comments, vote to rate this site, and also you can join us and many more.

Monday, November 19, 2012

Mishahara Serikalini Yapanda


Yapandisha mishahara ya vigogo ghafla
*Waziri adai imefuata taratibu
*Wengine waongezewa Sh milioni moja

SERIKALI imefanya marekebisho ya mishahara kwa watumishi wake kwa mwaka wa fedha 2012/2013, MTANZANIA imebaini. Sambamba na hilo, mishahara ya viongozi wa Serikali kwa mwaka huo wa fedha, nayo imefanyiwa marekebisho.

Marekebisho hayo ni kwa mujibu wa waraka wenye kumbukumbu namba S/AC 205/ 399/ 01/ 44, kutoka Ofisi ya Rais Ikulu (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), uliotolewa Julai 25, mwaka huu.

Waraka huo, umesambazwa kwa wakuu wote wa idara za Serikali, wakurugenzi wa majiji, manispaa, miji na wakurugenzi wa halmashauri zote za wilaya nchini.

Waraka huo, uliosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu (Utumishi), Hab Mkwizu, umehusisha pia marekebisho ya ngazi za mishahara kwa viongozi hao wa Serikali.

Kwa mujibu wa waraka huo, ngazi za mishahara zilizokuwa zinaanzia TGS I hadi TGS Q, zimebadilishwa na sasa zitasomeka LSS (E) 1 hadi LSS (E) 9.

Watumishi na viongozi wa Serikali walionufaika na marekebisho hayo, ni pamoja na makatibu wakuu wa wizara, manaibu wao pamoja na wakurugenzi wa idara zote za Serikali. Marekebisho hayo yameanza kutekelezwa Julai, 2012.

Hata hivyo, marekebisho hayo yamelalamikiwa na baadhi ya watumishi wa Serikali, wakidai kuwa hayana uwiyano unaoeleweka kati ya mishahara ya wamtumishi wa Serikali.

Marekebisho hayo yanaoneshwa katika kiambatanisho namba 1 cha waraka huo, ambapo watumishi na viongozi hao wameongezewa mshahara usiopungua 400,000.

Mfano mshahara wa mtumishi wa ngazi TGS P, umepanda kutoka Sh 3, 216, 000 hadi Sh 4, 500, 000 katika ngazi mpya ya LSS (E) 9, ongezeko ambalo ni zaidi ya Sh milioni moja.

Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikosoa marekebisho hayo na kusema kuwa, hayana uwiyano mzuri kati ya mshahara wa mtumishi na mtumishi mwingine.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani, amekiri kuwapo kwa marekebisho hayo ya mishahara kwa watumishi na viongozi wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Kombani alisema, marekebisho hayo ni ya kawaida na kwamba yanawagusa watumishi wote wa Serikali bila kubagua.

“Serikali ikifanya marekebisho ya mishahara, inafanya hivyo kwa watumishi wake wote. Hatuchagui nani aongezewe nani asiongezewe ni wote,” alisema.

Alisema vigezo vilivyotumika katika marekebisho hayo, ni pamoja na aina ya kazi, uzoefu na muda aliotumia mtumishi kukaa kazini.

“Unauliza kwanini watumishi wengine wamepewa nyongeza kubwa na wengine kidogo, ndugu yangu sifa zinatofautiana, mtumishi anayeanza kazi leo, hawezi kulipwa mshahara na mtumishi aliyepo kazini kwa miaka 20,” alisema.

Alipoulizwa ni sababu zipi zilizoifanya Serikali kurekebisha ngazi ya mshahara kutoka TGS na sasa kutumia ngazi mpya ya LSS, Waziri Kombani alisema. “Hayo ni masuala ya kitaalamu zaidi.”

Kombani alikiri kima cha chini cha mshahara ni kidogo na kueleza kuwa, Serikali ipo katika majadiliano.

“Kima cha chini kilipanda kutoka Sh 130, 000 hadi Sh 170, 000. Tunajua kima hiki hakitoshi lakini tupo katika majadiliano,” alisema.
Source: Mtanzania Jumatatu, Nov 19,2012

No comments:

Post a Comment